TRENDING NOW






Mkuu wa kitengo cha Mifumo Mbadala ya Kidijitali wa Benki ya Exim Bw. Silas Matoi, akizungumza na mmoja wa washindi wakati wa droo ya kwanza ya kampeni ya Chanja Kijanja, Dili ndio Hili iliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita. Kupitia kampeni hii, wateja wanaotumia kadi za Exim kulipia bidhaa au huduma wanapata nafasi ya kushinda zawadi ya pesa taslimu TZS 100,000 kila wiki, TZS 200,000 kila mwezi, pamoja na zawadi kubwa za TZS milioni 15, milioni 10 na milioni 5 mwisho wa kampeni.Kushoto ni Meneja Msaidizi wa Kitengo cha Mifumo Mbadala ya Kidijitali wa Benki ya Exim Benedict Mwinula, pamoja na Mkaguzi kutoka Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania, Rodgers Biteko (kulia), jijini Dar es Salaam.
Droo ya kwanza ya kampeni ya Chanja Kijanja, Dili ndio Hili imeibua washindi watano wa Sh. 100,000 kila mmoja! Mkuu wa Kitengo cha Mifumo Mbadala ya Kidijitali wa Benki ya Exim, Bw. Silas Matoi, aliwatangaza washindi huku akisisitiza kuwa hii ni mwanzo tu.

“Kila wiki, washindi watatangazwa, na kila mwezi washindi 10 watashinda Sh. 200,000. Vilevile, washindi wa droo kuu watapokea zawadi kubwa za Sh. milioni 5, milioni10, na mshindi mkuu Sh. milioni 15,” alisema Bw. Matoi.
Benedict Mwinula, Meneja Msaidizi wa Kitengo cha Mifumo Mbadala ya Kidijitali, pamoja na Rodgers Biteko, Mkaguzi kutoka Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania, walishiriki katika droo hii iliyofanyika mwishoni mwa wiki.

Kampeni ya Chanja Kijanja inalenga kuwapa wateja wa Exim fursa ya kushinda kila wanapotumia kadi za Exim kulipia bidhaa au huduma. Hii ni nafasi yako ya kuwa mmojawapo wa mshindi wa Sh. 15 milioni!
Na WMJJWM – Tunisia

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, ameshiriki Mkutano wa 6 wa Ngazi ya Juu kuhusu Masuala ya Wanawake, Amani na Usalama (WPS) uliofanyika tarehe 9–10 Desemba 2025 katika Chuo cha Kimataifa cha Diplomasia, jijini Tunis nchini Tunisia.

Akizungumza katika mkutano huo, Dkt. Gwajima ameupongeza Umoja wa Afrika kupitia Ofisi ya Mjumbe Maalum wa AU wa Masuala ya Wanawake, Amani na Usalama, pamoja na Serikali ya Tunisia kwa kuandaa mkutano huo muhimu wenye mstakabali wa Wanawake.

Akiwasilisha mchango wake katika mjadala wa jopo la wataalamu, Dkt. Gwajima amesema kasi ya ukuaji wa teknolojia na akili mnemba imekuwa na manufaa pale inapowezesha jamii kuelimishwa kuhusu madhara ya ukatili wa kijinsia, sambamba na kusambaza ujumbe wa kukataa vitendo hivyo.

Dkt. Gwajima pia ameeleza mafanikio makubwa yaliyofikiwa na Tanzania, ikiwemo kuzinduliwa kwa Mpango wa Taifa wa Kwanza wa Wanawake, Amani na Usalama (TNAP), mageuzi ya sera na sheria kama Sheria ya Uchaguzi ya 2024, pamoja na ongezeko la uwakilishi wa wanawake katika nafasi za maamuzi serikalini. Aidha, amebainisha hatua za serikali kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia mikopo ya asilimia 10 ya halmashauri na juhudi za kitaifa za kupambana na ukatili wa kijinsia.
Amesema mkutano huo unatoa fursa ya kutathmini mafanikio ya utekelezaji wa Ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama, pamoja na kubainisha changamoto na mikakati mipya ya kuimarisha utekelezaji wake barani Afrika.

Dkt. Gwajima ameeleza kuwa licha ya hatua nzuri zilizopigwa katika kupanua usawa wa kijinsia, wanawake bado wanakabiliwa na vikwazo mbalimbali huku akitaja mila na desturi kandamizi, changamoto za kiuchumi na athari wanazokutana nazo wanawake wanaojitokeza kugombea nafasi za uongozi kuwa miongoni mwa mambo yanayopunguza ushiriki wao katika uongozi na siasa.

Amesisitiza kuwa utekelezaji wenye tija wa ajenda ya WPS unahitaji ushirikiano mpana kati ya serikali, mashirika ya kiraia, wadau wa maendeleo na taasisi za kikanda huu akisema Tanzania itaendelea kushirikiana na Umoja wa Afrika na wadau wengine ili kuhakikisha wanawake wanapata nafasi stahiki katika meza za maamuzi na michakato ya ujenzi wa amani barani Afrika.

Hata hivyo, ameonya kuwa teknolojia hiyo hiyo imekuwa ikichochea aina mpya za ukatili wa kijinsia mtandaoni, ambao waathirika wakubwa ni wanawake na wasichana.

Amefafanua kuwa mitandao ya kijamii imekuwa ikitumika kusambaza video za uongo, chuki, vitisho na matusi yanayolenga kuwachafua wanawake hadharani, jambo linalotishia usalama wao mtandaoni na kuwavunja moyo wanaotaka kushiriki katika uongozi na siasa.

Aidha amehimiza wadau wote kushiriki kikamilifu katika kutoa hamasa na elimu juu ya matumizi salama ya mitandao ili kulinda wanawake, wasichana na jamii kwa ujumla.

Dodoma, Tanzania – 12 Desemba 2025

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Mbunge wa Jimbo la Peramiho, Mhe. Jenista Joakim Mhagama, kilichotokea jijini Dodoma.

Kupitia taarifa yake, Rais Samia amesema amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba huo mzito na kutoa pole kwa Spika wa Bunge, Mhe. Mussa Azzan Zungu, wananchi wa Jimbo la Peramiho, familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki.

Rais Samia amemuelezea Marehemu Mhagama kama kiongozi shupavu na mtumishi wa umma aliyejitoa kwa moyo wake wote kwa kipindi cha zaidi ya miaka 38 ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Katika safari yake ya kisiasa, Mhagama aliwahi kuwa kiongozi wa vijana, kiongozi wa wanawake, waziri katika awamu mbalimbali za serikali, pamoja na kuwa mshauri wa wanasiasa na wananchi wengi.

“Kwa miaka 38, Mheshimiwa Mhagama amekuwa mwanachama mahiri wa CCM, kiongozi wa vijana, kiongozi wa wanawake, waziri katika awamu mbalimbali na mnasihi wa wengi katika siasa na maisha,” amesema Rais Samia katika salamu zake.

Rais Samia amewaombea wafiwa faraja katika kipindi hiki cha majonzi na kumkabidhi marehemu kwa Mungu, akisema: “Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Amina.”

Mipango ya mazishi inaratibiwa kwa ushirikiano kati ya Serikali, Bunge na familia ya marehemu, na taarifa zaidi zinatarajiwa kutolewa.

Dodoma, 11 Desemba 2025

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limetangaza kifo cha Mbunge wa Peramiho, Mhe. Jenista Joakim Mhagama, kilichotokea leo jijini Dodoma. Taarifa hiyo imetolewa na Spika wa Bunge, Mhe. Mussa Azzan Zungu (Mb), kupitia taarifa rasmi ya Ofisi ya Bunge.

Katika taarifa hiyo, Spika Zungu alieleza kusikitishwa na msiba huo mzito, akisema:

“Kwa masikitiko makubwa, naomba kutangaza kifo cha Mbunge wa Peramiho, Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama kilichotokea leo 11 Desemba 2025 jijini Dodoma. Natoa pole kwa Waheshimiwa Wabunge wote, familia ya marehemu, ndugu, jamaa na wananchi wa Jimbo la Peramiho. Mwenyezi Mungu awape moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu.”

Ofisi ya Bunge imesema kuwa mipango ya mazishi itaendelea kutolewa kwa ushirikiano na familia ya marehemu.

Mhe. Jenista Mhagama alizaliwa tarehe 23 Juni 1967 na amehudumu katika nyadhifa mbalimbali za uongozi nchini, ikiwemo kuwa Mbunge na Waziri katika wizara tofauti.

Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Amina.